Ni Machi, 18, 2022 ambapo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anazungumza na vyombo vya habari muda huu.
“Mbowe aliyeingia gerezani ndo Mbowe aliyetoka gerezani, tena pengine akiwa imara zaidi. Kwa hiyo nimezungumza na Rais mambo kadhaa. Lakini sikuyafikisha kwa umma kwa sababu nilihitaji kwanza kuzungumza na Kamati Kuu ya Chama changu na viongozi wenzangu”– Mbowe
“Nilipokwenda gerezani, chama hiki hakikuenda gerezani. Viongozi wenzangu walikuwepo, vikao vya chama vilifanyika, mashauriano mbalimbali yalitokea. Ninaporejea kutoka gerezani ninapaswa kwanza kukabidhiwa kiti changu ndo nizungumze kama msemaji mkuu wa chama.”- Mbowe
“Kwa hiyo nawashukuru viongozi wenzangu walikilinda chama chetu katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo ilinipasa mimi kwanza nizungumze na kamati kuu ya chama changu ili nitakapotoa kauli kwa umma nitoe kauli ya chama na sio kauli ya Mbowe.”- Mbowe
“Waheshimiwa viongozi, nilipokwenda kukutana na mheshimiwa Rais Ikulu, tulichokizungumza ni kitu kimoja tu cha msingi. Kwamba tulikubaliana kutafuta njia za haki, za mazungumzo, za mashauriano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu.”- Mbowe
“Hatukuenda kuzungumza hoja yoyote, moja baada ya nyingine. Kwamba nchi hii tukubaliane ni yetu sote, wao wapo kwenye uongozi na utawala wa taifa, sisi ni chama kikuu cha upinzani, na kuna watanzania wengine ambao sio wanachama wa vyama hivi lakini ni watanzania wenzetu.” – Mbowe
“Na tulikubaliana kwamba tuna tatizo moja kubwa la kutokuaminiana kwa sababu tumekuwa na urafiki wa mashaka. Tumekua na urafiki wa mashaka na hakika tuna urafiki wa mashaka, hatuaminiani.”- Mbowe
“Tukakubaliana, ili kuvuka kikwazo hicho, lazima kila upande ujaribu kujenga kwa mwenzake, na majibu yatapatikana kwa wakati, sio jambo au tukio la siku moja. Hilo lilikua la kwanza la msingi.”- Mbowe