Mshambulizi huyo wa zamani wa Sunderland na Stade Rennes anastaafu kama mfungaji bora wa muda wote wa Ghana akiwa na mabao 51 pamoja na mchezaji wa pili wa nchi yake kucheza mechi nyingi zaidi.
“Ni wakati wa kutundika jezi na buti kwa heshima ninapostaafu rasmi kutoka kwa kandanda.’‘ Gyan alisema katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Mshambuliaji huyo alifunga mabao 51 katika mechi 109 alizoichezea nchi hiyo, na kumfanya kuwa mfungaji bora wa Ghana.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 alianza soka ya klabu mwaka 2003 akiichezea timu ya kwanza ya Ghana, Liberty Professionals, na baadaye akacheza Ulaya katika klabu za Udinese ya Serie A ya Italia, Rennes ya Ligue 1 ya Ufaransa na Sunderland ya Ligi Kuu ya Uingereza, ambapo alivunja rekodi ya uhamisho wa klabu hiyo.
Aliwahi kucheza katika Milki ya Falme za Kiarabu, akiichezea Al Ain, akiisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi ya UAE na kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa amefunga mabao 28 katika mechi 32.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 pia hakujumuishwa kwenye kikosi cha Ghana kwa ajili ya Kombe la Dunia mwaka jana, huku Black Stars wakitoka katika michuano hiyo katika hatua ya makundi.
Katika ngazi ya klabu, mara ya mwisho aliichezea Legon Cities inayoshiriki Ligi Kuu ya Ghana miaka miwili iliyopita, lakini hajacheza tangu walipoachana nao.