MSHAMBULIAJI wa Yanga, Emmanuel Okwi, amefurahi kuanza na bao kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara akiwa na timu hiyo huku straika, Didier Kavumbagu, akipagawa na makali ya fowadi yao.
Yanga iliipiga Ruvu Shooting mabao 7-0 juzi Jumamosi ikiwa ni siku chache baada ya kuiondosha Komorozine ya Comoro kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 12-2.
Okwi ambaye katika ushindi dhidi ya Ruvu Shooting alipiga bao moja, alisema: “Ninavyoona morali ya wachezaji wenzangu, sidhani kama kuna timu inaweza kutuzuia kwa sasa, ngoja twende kambini tukajiandae na mchezo ujao (dhidi ya Ahly wa Ligi ya Mabingwa) hatuwezi kuiogopa timu yoyote kwani kikosi chetu kipo imara.”
Katika mchezo huo, Okwi alipiga pasi za maana zaidi ya 28. Alipiga mashuti mawili yote yakilenga lango na kichwa kimoja huku akionyesha uelewano mkubwa na Simon Msuva, Hamis Kiiza, Kavumbagu na Mrisho Ngassa.
Kavumbagu kwa upande wake alisema mabao hayo waliyoifunga Ruvu Shooting, ni salamu kwa timu nyingine yoyote watakayokutana nayo, kutokana na kikosi chao cha kwanza kuundwa na viungo washambuliaji wenye kasi ya aina yake.
“Kurejea kwa Okwi kumeimarisha kikosi chetu katika safu ya ushambuliaji inayoundwa na wachezaji wote wenye uwezo mkubwa ndani ya uwanja, hali hii inanipa matumaini ya kuendelea kupata ushindi wa mabao mengi katika kila mechi,” alisema Kavumbagu ambaye ni raia wa Burundi.
Mshambuliaji Hamis Kiiza, alisema: “Hizo ni salamu kwa wapinzani wetu wote kuanzia kwenye Ligi Kuu na hata kimataifa, lazima waweke hofu dhidi yetu na hilo ndilo linalotakiwa, hatutakubali kushuka kwenye kiwango hiki kwani lengo letu ni kutwaa ubingwa wa Bara na hata kufanya vizuri kimataifa.”
Source: Mwanaspoti