Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2019, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amepokea tuzo hiyo mjini Oslo, Norway huku akionya dhidi ya mataifa yenye nguvu za kijeshi na makundi ya waasi yanayohatarisha usalama kwenye eneo la Pembe ya Afrika.
Abiy alishinda tuzo hiyo mwezi Oktoba kutokana na jitihada zake za kusaka amani zilizohitimisha miongo miwili ya uhasama kati ya nchi yake na Eritrea, amesema tuzo hiyo pia ni kwa ajili ya kiongozi wa Eritrea, Isaias Afwerki.
Kiongozi huyo amesema amepokea tuzo hiyo pia kwa niaba ya kiongozi wa Eritrea, ambaye nia yake njema pamoja na kujitolea kumewezesha kukomesha kwa miongo miwili ya mkwamo baina ya nchi hizo.
Aidha pia Mshindi huyo wa Nobel pia amesema ameipokea tuzo hiyo pia kwa niaba ya Waafrika na Ulimwengu wote ambao ndoto zao za kuwa na amani kila siku zimegeuzwa kuwa jinamizi la vita.
Tangu alipoingia madarakani mwaka jana Abiy ameongoza mageuzi makubwa ya kisiasa ambayo yamempatia heshima kubwa ndani na nje ya nchi hiyo, lakini pia yamefunguwa njia kwa mizozo ya ndani ya kikabila.