NIPASHE
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amekanusha uvumi kuwa ana mpango wa kujiunga na Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT)-Tanzania.
Kafulila amesema hana mpango wa kuachana na chama chake na taarifa zilizopo ni za kizushi; “Hizo taarifa zitaendelea kuwa za tetesi tu, mimi bado mwanachama wa NCCR-Mageuzi na sina mpango wowote wa kujiunga na chama chochote cha siasa kwa sasa wala kwa baadaye,” David Kafulila.
Mbunge huyo amesema kwa sasa anaendelea kufanya kazi za jimbo na ana uhakika wa kurudi bungeni kwa mara nyingine kuwawakilisha wananchi wa Kigoma Kusini kupitia chama cha NCCR-Mageuzi na si chama kingine cha kisiasa.
Miongoni mwa waliojiunga na chama hicho cha ACT-Tanzania ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Arusha, Samson Mwigamba pamoja na Zitto Kabwe ambao walisimamishwa pamoja na Prof. Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA.
Wiki iliyopita Mbunge Halima Mdee na John Shibuda, wote wa CHADEMA, walikanusha Bungeni kuhusishwa na mipango ya kujiunga na ACT Tanzania.
NIPASHE
Watu watano wamefariki Wilaya ya Chato, Geita baada ya kupigwa na radi wakati wakiendelea na ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Assemblies of God Tanzania.
Katika ajali hiyo watu wengine 18 walijeruhiwa na wanne kati yao bado wamelazwa katika Zahanati ya Bwanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo akizungumza na NIPASHE alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliofariki pamoja na majeruhi wa tukio hilo.
Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Deogratias John alisema majeruhi 18 walipokelewa katika lakini 14 walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata nafuu.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa kata hiyo, Mahobe Chiza alisema; “Walikuwa katika sikukuu ya Pasaka, lakini bahati mbaya mvua iliyokuwa ikinyesha ilisababisha radi kupiga na kuwadhuru waumini hao”
“Kila nafsi itaonja mauti, lakini tukio hili limewaachia simanzi kubwa waumini wa kanisa pamoja na wananchi kutokana na kupotea kwa nguvu kazi ya kanisa na taifa kwa ujumla,” alisema Mchungaji wa kanisa hilo, Deus Mhangwa.
TANZANIA DAIMA
Tangu kuanza kwa mwaka huu 2015 kumekuwa na matukio mengi ya Askari wa Jeshi la Polisi kujiua kwa kujipiga risasi huku uchunguzi uliofanywa na gazeti la TANZANIA DAIMA ukionesha kuna tukio la Askari mmoja kujiua kila mwezi.
Tukio la kwanza la Askari kujiua 2015 lilitokea Januari 6 Mbozi, Mbeya, likafuatia tukio jingine February 3 ambapo aliyekuwa dereva wa OCD wa Manyoni alijiua kwa kujipiga risasi mdomoni ambapo bastola aliyoitumia aliiomba katika ghala la silaha akidai kuwa na safari ya kikazi na Bosi wake.
Tukio jingine lilitokea Machi 18 Askari mwingine alijiua Kagera alijiua kwa kujipiga risasi akiwa lindoni katika Tawi la Benki, chanzo cha kujiua haikufahamika.
April 4 mwaka huu Askari Polisi mmoja Sikonge, Tabora alijiua kwa alijipiga risasi usiku akiwa kituo cha Polisi ambae nae sababu ya kujiua haijafahamika mpaka sasa.
Inadaiwa kuwa Askari hao kabla ya kutekeleza vitendo hivyo wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha.
MWANANCHI
Wakati makundi mbalimbali yakipigana vikumbo kumshawishi aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo agombee urais, mwenyewe amesema muda bado, ukifika atasema.
Baadhi ya makundi yaliyojitokeza na kumtaka agombee ni Chama cha Watu wenye ulemavu mkoani Mwanza na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Jomo Kenyatta, IAA, Semmco na Makumira.
Akiwa bungeni Dodoma, Prof. Muhongo amekuwa akitajwa na wabunge wenzake kama rais mtarajiwa, alipoulizwa na gazeti la NIPASHE kuhusu suala hilo, alijibu “Ya kwangu nitayasema muda ukifika.”
Alisema kama kuna watu wanamuunga mkono hawezi kuwazuia, ila wasiandamane kumfuata kwa nia ya kumshawishi kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.
Prof. Muhongo alisema kuwa ni mapema sana kuzungumza kama atawania urais au la.
“Hawajaja (wanafunzi) kuniona kama wanataka (kunishawishi) waendelee huko huko si kuja kwangu.. Taratibu zimewekwa mbona mnakuwa na wasiwasi, ya kwangu nataka nikiyaongea muda uwe umefika,” alisema Prof. Muhongo.
MWANANCHI
Hospitali ya Wilaya Kondoa imeingia kwenye kashfa baada ya kubainika kuwa wajawazito wanaokwenda kupata matibabu wanalazimishwa kufanya usafi wodini na chooni katika Hospitali hiyo.
Taarifa kutoka Hospitalini hapo zimedai kwamba utaratibu huo umekuwepo kwa muda mrefu ambapo wanawake hao wamejikuta wakilazimika kutii na kuufuata utaratibu huo kwa muda wote.
“Mimi nimekuja kujifungua kwa bahati mbaya mambo hayajawa tayari, nimeonekana nina matatizo lakini nimefika hapa nimepangiwa zamu ya usafi, unafikiri nawezaje kukataa katika hali hii? Nalazimika kufanya ili mradi siku yangu ikifika ya kujifungua nijifungue salama, nikibisha nahofia naweza nikanyimwa huduma”—aliongea mmoja wa wagonjwa hao.
Mwandishi wa gazeti la NIPASHE alifika Hospitali hapo kwenye Wodi ya akina mama na kukuta harufu mbaya ya choo na bafu pamoja na mashuka kwenye vitanda kuwa machafu.
“Ni kweli wanafanya usafi lakini sio kwa kiasi hicho wanachodai.. kwani kuna tatizo mtu kufanya usafi pale anapoishi? Maana wodini ni sawa na nyumbani kwao”—alijibu Mganga Mkuu msaidizi wa Wilaya hiyo, Abdallah Othman, na kuongeza kuwa hiyo ni sehemu ya mazoezi ya kuwaweka kwenye hali nzuri.
Kaa karibu na millardayo.com nitakachokipata nitakusogezea hapa muda wowote kuanzia sasa, unaweza kujiunga na mimi kwenye Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge hapa >>>twitter Insta Facebook