Zaidi ya Polisi 3,000 na Maofisa wengine wa usalama wa Ufaransa waliuzunguka Mji Mkuu wa Ufaransa Paris jana Jumamosi ikiwa ni jumamosi ya tatu ya maandamano wakati maelfu ya Waandamanaji wakipinga mpango wa Serikali wa kuanzisha passport au pasi maalumu itakayokua ikitumika na waliopata chanjo dhidi ya virusi vya corona tu.
Nchini kote Ufaransa, Watu wapatao 204,000 wameshiriki maandamano hayo ambapo idadi hiyo ya Waandamanaji imeongezeka ikilinganishwa na ile ya wikiendi iliyopita, ndani ya Paris Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya Waandamanaji katika mikusanyiko minne tofauti mjini humo.
Kuanzia Agosti 9 pasi hizo mpya za afya zitahitajika kwa Raia kuweza kusafiri na kuingia kwenye maeneo ya biashara, kama vile migahawa, vinyozi, pamoja na kupanda kwenye treni au kushiriki kwenye maonyesho tofauti, pendekezo hilo bado linasubiri idhini ya kupitishwa na Baraza la Katiba ambapo itafanya upigaji wa chanjo hiyo ya virusi vya corona kuwa lazima kwa baadhi ya Wafanyakazi.
Maambukizi ya corona yaliyotokana na aina mpya ya kirusi iitwayo Delta yameongezeka nchini Ufaransa ambapo kwa Ijumaa pekee kumeripotiwa maambukizi mapya ya Watu 24,000 huku utafiti ukionesha kuwa Watu ambao bado hawajapata chanjo ni asilimia 85 ya wanaougua COVID-19 hospitalini ikiwa ni pamoja na wale waliolazwa kwenye vyumba vya kutunza wagonjwa mahatuti.
Watu wapatao 112,000 wamefariki dunia Ufaransa kutokana na virusi vya corona tangu janga hilo kuanza mwaka jana na hadi sasa asilimia 52 ya Watu wa Ufaransa wameshachanjwa.