Tarehe 19/12/2022 yamefanyika makabidhiano ya vifaa vya Tehama kwaajili ya Maabara za Hospitali za Rufaa za Kanda ikiwemo Bugando, KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya.
Vifaa hivyo vya Tehama zikiwemo Kompyuta, Viyoyozi, Printa na vifaa vingine venye thamani ya jumla ya Shilingi Bilioni 1, vinategemewa kwenda kuboresha utoaji wa huduma za maabara katika Hospitali tatu za Rufaa za Kanda kwa Tanzania bara.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amebainisha kuwa vifaa hivyo ambavyo vimetokana na fedha zilizotolewa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kupitia Shirika la PATH, vitakwenda kusaidia utoaji huduma za Maabara katika Hospitali za Rufaa nchini kupitia mifumo itakayowekwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi za Maabara.
Aidha Prof. Abel Makubi amewataka watakaopewa vifaa hivyo kuhakikisha wanasimamia matumizi na kufanya uchunguzi kila baada ya miezi sita utakaosaidia kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa matumzi yake.