WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea magari 51 ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa msaada wa dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii Tanzania katika hifadhi za Taifa Serengeti, Nyerere na Pori la Akiba Selous wenye thamani ya Euro milioni 20 sawa na shilingi BILIONI 56.
Mradi huo unahusisha ununuzi wa magari zaidi ya 60, ndege moja na helikopta moja kwa ajili ya kuimarisha doria, uanzishwaji wa benki za uhifadhi za jamii pamoja na kuboresha mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji 55 vinavyozunguka ya hifadhi hizo.
Majaliwa amepokea msaada huo wa magari 51 kutoka Serikali ya Ujerumani leo katika hafla iliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali ya Tanzania inathamini na kutambua uungwaji mkono na Serikali ya Ujerumani kupitia Msaada wa Dharura wa uboreshaji wa shughuli za Uhifadhi wa Utalii ambao utekelezaji wake ulisainiwa Oktoba 2021 na unatekelezwa kwa pamoja kati ya TANAPA, TAWA na shirika lisilo la Kiserikali la Frankfurt Zoological Society (FZS) kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na kueleza kuwa magari hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba wa vitendea kazi.
“Nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi na Wakuu wa Mashirika ya TANAPA na TAWA kuhakikisha msaada huu wa vitendea kazi unaenda kufanya kazi zilizokusudiwa za uhifadhi wa maliasili na utalii na kwamba vitendea kazi hivi vitumike na kutunzwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya matumizi ya mali za Serikali.”