LEO Juni 06, 2023, Waziri wa sanaa, Utamaduni na michezo, Pindi Chana anawasilisha Bungeni Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ya Wizara hiyo.
Hizi ni baadhi ya picha za Wasanii waliofika Bungeni hapo kwaajili ya kusikilisha hotuba hiyo inayowasilishwa na Waziri Pindi Chana
‘Kwa upande wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ni Shilingi Bilioni Tano, Milioni Mia Tatu Tisini na Sita, Mia Nne Hamsini na Tano Elfu (Shilingi 5,396,455,000) ambapo shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Tisa Tisini na Nane, Mia Tatu Kumi na Tano Elfu, Mia Sita Kumi na Moja (Shilingi 2,998,315,611) sawa na asilimia 55.5 ya lengo zilikuwa zimekusanywa hadi kufikia mwezi Aprili, 2023’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Miongoni mwa sababu zilizochangia kutofikiwa malengo ni kutokana na wadau wengi wa filamu kufanya kazi zao bila ya kufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kukosa vibali na kuingiza filamu sokoni kabla ya kuhakikiwa; na kuchelewa kukusanywa na kugawanywa kwa mirabaha ya kazi za wabunifu. Fauka ya hayo, kwa upande wa vyuo, moja ya sababu ni wanavyuo kutokulipa ada kwa wakati kutokana na changamoto mbalimbali’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Katika mwaka wa fedha 2022/23, Wizara iliidhinishiwa bajeti yenye jumla ya Shilingi Bilioni Thelathini na Tano, Milioni Mia Nne Ishirini na Tano, Mia Tisa Tisini na Moja Elfu (Sh. 35,425,991,000) ambapo kati ya hizo Mishahara ilikuwa Shilingi Bilioni Nane, Milioni Mia Mbili na Moja, Mia Nane Themanini na Mbili Elfu (Sh. 8,201,882,000), Matumizi Mengineyo (OC) shilingi Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia Tatu Tisini na Mbili, Mia Tisa Arobaini na Tisa Elfu (Sh. 11,392,949,000) na Miradi ya Maendeleo (DEV) Shilingi Bilioni Kumi na Tano, Milioni Mia Nane Thelathini na Moja, Mia Moja Sitini Elfu (Sh. 15,831,160,000)’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
“Katika kutekeleza azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza Kiswahili kimataifa, BAKITA limeandaa na kusambaza vitabu vya ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani” – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo #BajetiyaBurudani2023
“Hadi kufikia mwezi Aprili, 2023 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi Bilioni Ishirini na Nane, Milioni Mia Moja Sitini na Moja, Mia Tisa Thelathini na Nne Elfu, Mia Saba Sabini na Moja (Sh. 28,161,934,771) sawa na asilimia 79.5 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha zilizopokelewa, Shilingi Bilioni Tisa, Milioni Mia Tano Sitini na Moja, Mia Tatu Themanini Elfu, Mia Tisa Tisini na Tisa (Sh. 9,561,380,999) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo ya Wizara na Taasisi sawa na asilimia 83.9 ya bajeti ya Matumizi Mengineyo; Shilingi Bilioni Sita, Milioni Mia Saba Sabini na Mbili, Mia Tatu Tisini Elfu, na Themanini na Moja (Sh. 6,772,390,081) ni Mishahara ya Wizara na Taasisi sawa na asilimia 82.5 ya bajeti ya Mishahara; na Shilingi Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia Nane Ishirini na Nane, Mia Moja Sitini na Tatu Elfu, Mia Sita Tisini (Sh. 11,828,163,690) ni Miradi ya Maendeleo ambayo sawa na asilimia 74.7 ya bajeti ya Miradi ya Maendeleo’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Katika kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanaendelea kunufaika na utamaduni wao, Wizara iliratibu Tamasha kubwa la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 3 Julai, 2022 Jijini Dar es Salaam. Tamasha hilo lilitoa fursa kwa wananchi wetu kufanya matembezi ya kiutamaduni, mashindano ya ngoma za asili, maonesho ya vyakula vya asili, maonesho ya kazi za mikono za kiutamaduni na ubunifu pamoja na kuuza kazi hizo. Jumla ya vikundi 24 vya ngoma za asili kutoka mikoa ya Tanzania Bara na vikundi viwili (2) kutoka mikoa miwili (2) ya Zanzibar vilishiriki katika Tamasha hilo’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Kushirikiana na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni ya Jamhuri ya Afrika Kusini inaendelea na maandalizi ya Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania linalotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2023. Lengo la Tamasha hilo ni kutangaza kazi za Sanaa, Utamaduni, ubunifu kimataifa na asili ya Mtanzania na utamaduni wake’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani
‘Kiswahili imekuwa Lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ni Lugha rasmi na ya Kazi ya Umoja wa Afrika (AU). Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya lugha hii, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limepitisha tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, ambayo kwa mara ya kwanza ilisherehekewa tarehe 7 Julai, 2022’ – Pindi Chana, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo #BajetiYaBurudani