Mwili wa aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza unazikwa leo kwenye makaburi ya Mji wa Gitega (Mji mkuu wa Kisiasa) uliopo katikati ya Burundi.
Hafla ya mazishi inatarajiwa kuongozwa na Rais mpya, Jenerali Evariste Ndayishimiye na wakuu wengine wa serikali.
Rais Pierre Nkurunziza alifariki dunia tarehe 8 kutokana na mshtuko wa moyo kama ilivyotangazwa na serikali ya nchi hiyo, ikiwa ni miezi miwili kabla ya kukabidhi madaraka kwa mrithi wake kufuatia uchaguzi uliofanyika mwezi Mei.
Taarifa kutoka Serikali ya Burundi inasema, hafla itaanzia kwenye hospitali ijulikanayo kama ‘hospital du Cenquantenaire Twese Turashoboye’ iliyoko kwenye mkoa wa Karusi ambako mwili wake umehifadhiwa.
Magari yatakayosindikiza mwili wake yataanzia kwenye hospitali hiyo na kuelekea katika mji wa Gitega ambao ni mji mkuu wa kisiasa katikati mwa Burundi.
Wananchi wameomba kusimama kwenye barabara kumuaga Nkurunziza.
Hafla fupi ya jeshi kumtolea heshima za mwisho kwenye uwanja wa mpira wa Ingoma mjini Gitega itafuata, kabla ya mwili wake kupitishwa mbele ya wananchi watakaokuwa uwanjani humo kumwaga na baadae kufanyika maziko rasmi.
Tangazo la serikali ya Burundi linasema kwamba shughuli nyingine kama kuweka mashada ya maua kwenye kaburi lake au hotuba zitafuata utaratibu maalum.