Kesi iliyokuwa ikimkabili mwanariadha wa nchini Afrika Kusini, Oscar Pistorius hatimaye imefikia ukingoni ambapo Mahakama ya jijini Pretoria imemkuta na hatia ya mauaji ya bila kukusudia.
Kutokana na kukutwa na hatia hiyo, mahakama ikiongozwa na jaji Thokozile Masipa imeamuru Pistorius atumikie kifungo cha miaka 5 jela.
Wakati wa kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, ndugu wa Pistorius walionesha kukata tamaa japo waliahidi kusimama pamoja na Pistorius bila ya kujali hukumu gani itaamriwa na mahakama hiyo.
Mwanariadha huyo amekutwa na hatia hiyo baada ya kushitakiwa kwa kesi ya kumuua kwa kumpiga risasi aliyekuwa mchumba Wake, Reeva Steenkamp tarehe 14 Februari, 2013.
Kwa mujibu wa ripota wa BBC, aliyeshuhudia tukio zima la kutolewa kwa hukumu hukumu hiyo amesema, wazazi wa Steenkamp wameonesha kuridhishwa na hukumu hiyo na wanaamini kesi imekwisha.
Mwanasheria wa familia ya Steenkamp, Dup De Bruyn ameongeza kuwa hukumu iliyotolewa mahakamani hapo imezingatia haki.
Wakili wa Pistorious amesema alitegemea mteja wake atahukumiwa kifungo cha miezi 10, pamoja na kifungo cha nje, na si kama mahakama hiyo ilivyoamua.
Pistorius anaanza kutumikia kifungo hicho huku baadhi ya wanasheria nchini humo wakisema kuwa bado mwanariadha huyo ana nafasi ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.