Rais Magufuli amepokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2017/18 iliyowasilishwa kwake na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Diwani Athumani.
Katika taarifa hiyo Kamishna Diwani Athumani amesema TAKUKURU imepata mafanikio katika kuzuia na kupambana na rushwa katika mwaka 2017/18 na ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuokoa fedha za Serikali kiasi cha Bilioni 70.3 ambazo zingepotea kutokana na vitendo vya rushwa, kurudisha Bilioni 13.1 zilizotokana na matukio ya ukwepaji wa kodi na kesi kubwa 3 za wakweji wa kodi ambazo kufunguliwa katika Mahakama Kuu kitengo cha rushwa na uhujumu uchumi zenye thamani ya shilingi Bilioni 27.7.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kesi za rushwa zilizofunguliwa katika mahakama mbalimbali kutoka kesi 435 za mwaka 2016/17 hadi kesi 495 ambapo kati yake kesi 296 zimeamriwa na katika kesi 178 watuhumiwa wamepata adhabu ya vifungo mbalimbali, sawa na asilimia 60.1 ukilinganisha na asilimia 41 iliyofikiwa mwaka 2016/17.
Akizungumzia taarifa hiyo Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na timu yake kwa juhudi kubwa wanazozionesha katika mapambano dhidi ya rushwa na ameitaka taasisi hiyo kuendelea kufichua mianya yote ya vitendo vya rushwa nchini.
Ametoa mfano wa mianya hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa walipa kodi wenye mashine za kutolea risiti (EFD) zisizotambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), madai ya kughushi ya marejesho ya kodi (Tax Refunds) na ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara akiwemo mfanyabiashara mmoja aliyekwepa kulipa zaidi ya shilingi Bilioni 8.3 kutokana na kuingiza nchini magari 176.
Rais Magufuli pia amemtaka Kamishna Diwani Athumani kuhakikisha anawachukulia hatua wafanyakazi wa TAKUKURU ambao wanakiuka maadili ikiwemo kujihusisha na rushwa, akiwemo mtumishi mmoja ambaye anayedaiwa kujikusanyia zaidi ya shilingi Bilioni 1.4 kwa kuwauzia watumishi wa TAKUKURU viwanja hewa.
ASKARI ALIEMUOKOA FUNDI NDANI YA MV. NYERERE APANDISHWA CHEO