Jumla ya watuhumiwa 146 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo ujambazi na uhamiaji haramu zoezi ambalo lilifanyika wakati wa operesheni ya kutokomeza vitendo vya uhalifu ambalo lilianza mwezi uliopita.
Akizungumzia tukio hilo katika kituo kidogo cha polisi kilichopo kijiji cha Mvugwe wilaya Kasulu mkoani Kigoma mkuu wa opereshi maalumu Jeshi la Polisi Mihayo Msikhela amesema operesheni hiyo imehusisha ukamataji wa silaha za kivita za jadi pamoja na bangi.
Ameeleza tangu kuanza kwa oporesheni hiyo watu waliohusika katika matukio matatu likiwemo la mauaji ya mtu mmoja kutoka wilayani kasulu watuhumiwa wa matukio hayo wamekamatwa wakiwa na silaha za jadi pamoja na silaha za kivita.
Aidha akizungumzia tukio lingine amesema watu watano ambao ni Watanzania wamekamatwa kwa kosa la kuwahifadhi wahamiaji kutoka nchi jirani ya Burundi ambapo hapa anatoa wito kwa jamii kushirikiana na jeshi la polisi kutokomeza vitendo hivyo.