Kylian Mbappe, mshambuliaji mashuhuri wa Ufaransa, ameelezea wazi klabu yake ya sasa ya Paris St-Germain (PSG) kama “klabu yenye mgawanyiko,” na hivyo kuchochea uvumi kuhusu mustakabali wake na mabingwa hao wa Ufaransa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, ambaye mkataba wake na PSG unatamatika 2024, alielezea hisia zake wakati wa mahojiano na jarida la France Football.
Mbappe ameifahamisha klabu hiyo kwamba hatasaini mkataba mpya, jambo linalozua shaka kuhusu kujitolea kwake kwa muda mrefu PSG.
Kwa mujibu wa ripoti, Mbappe alisema, “Ninaamini kuwa kucheza PSG hakutoi mchango mkubwa kwa sababu ni timu na klabu inayoleta mgawanyiko.”
Kujibu msimamo huo wa Mbappe, mwenyekiti wa Paris St-Germain, Nasser Al-Khelaifi, ameweka wazi kuwa hatamruhusu mshambuliaji huyo mwenye kipaji kikubwa kuondoka kwa uhamisho wa bure mara tu mkataba wake utakapokamilika msimu ujao wa joto.
Akiwa amejiunga na PSG kutoka Monaco mwaka 2017, Mbappe amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.
Ameisaidia PSG kupata mataji matano ya Ligue 1, pamoja na ushindi wao wa hivi majuzi, na kufunga mabao 41 ya kuvutia katika mashindano yote msimu uliopita.
Hata hivyo, klabu hiyo mara kwa mara imekuwa ikishindwa kutimiza matarajio yao katika michuano ya UEFA Champions League, huku kampeni yao ikiishia katika hatua ya 16 bora dhidi ya Bayern Munich.
Akizungumzia uchezaji wa timu, Mbappe alisema, “Tulifanya tulichoweza. Ni muhimu kuzungumza na wale wanaounda timu, wanaounda kikosi, na wanaojenga klabu hii.”
Hivi majuzi PSG walimteua Luis Enrique kama kocha wao mkuu mpya akichukua nafasi ya Christophe Galtier. Enrique anachukua jukumu la kukinoa kikosi ambacho kinapitia kipindi cha mpito, kwani tayari PSG imeshuhudia kuondoka kwa mshindi wa Kombe la Dunia kutoka Argentina Lionel Messi kwenda Inter Miami. Zaidi ya hayo, mustakabali wa fowadi wa Brazil Neymar bado haujulikani.
Huku Kylian Mbappe akieleza waziwazi wasiwasi wake na PSG ikikabiliwa na mabadiliko makubwa ndani na nje ya uwanja, miezi ijayo inaahidi kuwa muhimu kwa mustakabali wa klabu hiyo na uwezekano wa kuondoka kwa Mbappe.