Shirika la habari la Associated Press linaripoti kwamba Putin amekutana na Yevgeny Prigozhin, kiongozi wa Wagner, siku chache baada ya uasi wa muda mfupi wa mkuu wa mamluki na jeshi lake la kibinafsi.
Kwa mujibu wa msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, mkutano wa saa tatu ulifanyika tarehe 29 Juni, ambao pia ulihusisha makamanda kutoka kampuni ya kijeshi ya Prigozhin iliyoanzishwa.
Prigozhin amekuwa na mzozo wa muda mrefu na wakuu wa kijeshi wa Urusi ambao mnamo Juni 24 uliishia kwa uasi wa kutumia silaha ambapo aliwaongoza wapiganaji wake nchini Urusi.
Mkuu wa kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, atahamia Belarus chini ya makubaliano ya kumaliza uasi wa kijeshi alioongoza dhidi ya uongozi wa kijeshi wa Urusi, Kremlin ilisema Jumamosi usiku.
Mkataba huo ulisimamiwa na rais wa Belarus Alexander Lukashenko.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Lukasjenko amejitolea kufanya upatanishi, kwa makubaliano ya Vladimir Putin, kwa sababu alimfahamu Prigozhin kibinafsi kwa takriban miaka 20.
Peskov alisema kesi ya jinai ambayo ilikuwa imefunguliwa dhidi ya Prigozhin kwa uasi wa kutumia silaha itafutwa, na kwamba wapiganaji wa Wagner ambao walishiriki katika “maandamano yake ya haki” hawatachukuliwa hatua yoyote, kwa kutambua huduma yao ya awali kwa Urusi.
Ingawa Putin aliapa awali kuwaadhibu wale walioshiriki katika maasi hayo, Peskov alisema makubaliano hayo yalikuwa na “lengo la juu” la kuepusha makabiliano na umwagaji damu.
Prigozhin na wapiganaji wake wote walihama makao makuu ya kijeshi katika mji wa kusini wa Rostov-on-Don ambao walikuwa wamechukua hapo awali, shirika la habari la RIA liliripoti.