Wachezaji wa timu ya taifa ya Hispania wamewasihi mashabiki wao kuacha kumzomea beki wa klabu ya Barcelona na timu hiyo, Gerard Pique ambaye hivi karibuni amejikuta akiingia kwenye utata mkubwa na mashabiki wa Hispania.
Pique amekuwa akizomewa na kutukanwa na mashabiki wa Hispania kwenye mechi za timu hiyo zinazochezwa nchini Hispania na hali hiyo ilijitokeza zaidi katika mchezo wa mwisho ambao vijana wa Vincente Del Bosque walicheza kwenye uwanja wa Carlos Tartierre dhidi ya Slovakia.
Wachezaji waandamizi kwenye timu ya taifa ya Hispania wakiongozwa na Andres Iniesta na nahodha Iker Casillas kwa nyakati tofauti wamejitokeza na kuwataka mashabiki kuacha kumzomea Pique kwani wakifanya hivyo wanamvunja moyo.
Jordi Alba na Pedro Rodriguez nao wameingilia kati suala hili wakisema kuwa Pique ni mchezaji ambaye amejitolea kwa ajili ya taifa lake na anapswa kushangiliwa na kuungwa mkono badala ya kuzomewa.
Kocha wa timu ya taifa Vicente Del Bosque naye alimetea mchezaji wake akisema kuwa haelewi kwanini Pique anazomewa na mashabiki wakati siku zote amekuwa akicheza vizuri kwa kujituma na kupambana awapo uwanjani.
Hata hivyo nahodha wa Hispania Iker Casillas alikuwa mwanadiplomasia zaidi ambapo hakutaka kumtetea Pique moja kwa moja au kuwashutumu mashabiki na badala yake alisema kuwa yeye na wenzie kama timu watajaribu kumsahihisha Pique katika makossa na mienendo yake ili kuboresha uhusiano wake na mashabiki.
Katika siku za hivi karibuni Pique ameonekana kuwakera mashabiki kwa vitendo kadhaa ambavyo amekuwa akivifanya , Pique alianza kuwaudhi mashabiki kwa kuhudhuria mkutano wa hadhara ulioitishwa na wanasiasa wanaopigania uhuru wa jimbo la Catalunya huku akitoa maneno ya kusifu mkutano huo.
Zaidi ya Hapo Pique alionekana kuwauna mkono mashabiki waliozomea wimbo wa taifa kwenye mchezo wa fainali ya kombe la Copa Del Rey na amewakera mashabiki wa Real Madrid pia kwa maneno kadhaa ya kashfa dhidi ya timu yao.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos