Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika, Mkuu wa Nchi ya Comoro Azali Assoumani alipaswa kuzuru Mali na Burkina Faso kuanzia Agosti 14. Lakini ziara hiyo imeahirishwa, kwa sababu ya mabishano kuhusu picha iliyopigwa wakati wa mkutano wa kilele wa Urusi naAfrika ambao ulifanyika kati ya Julai 26 na 29 huko Saint Petersburg.
Kesi hiyo ilianza Julai 27, ambapo baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika, akiwemo wa Comoro anayeshikilia kiti cha urais wa Umoja wa Afrika, waliamua kususia kupiga picha ya marais katika mkutano huo wa Saint Petersburg. Sababu: uwepo hasa wa viongozi wa Mali na Burkina Faso, walioingia madarakani baada ya mapinduzi.
Uamuzi ambao umepingwa na Bamako na Ouagadougou kwa kulipiza kisasi, marais Assimi Goïta wa Mali na Ibrahim Traoré wa Burkina Faso wameamua kumtaja Azali Assoumani kuwa ni mtu asiyefaa na hatakiwi katika nchi zao. Ziara hii, ambayo lengo lake lilikuwa kutathmini kalenda ya uchaguzi nchini Mali na Burkina Faso kwa nia ya kurejea kwa utaratibu wa kikatiba, kwa hivyo haitafanyika.
Akihojiwa na RFI, Houmed Msaidié, msemaji wa serikali ya Comoro, amekumbusha kuwa rais Azali ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika mwaka huu, ambao unapinga vikali mapinduzi. Bado kulingana na yeye, tawala hizi za kijeshi ziko chini ya vikwazo vya ECOWAS, Umoja wa Afrika na kimataifa, picha hii ya viongozi haikuwezekana.
Msemaji huyo pia amekariri kwamba kurejea kwa utaratibu wa kikatiba katika nchi hizi mbili bado ni kipaumbele cha rais wa Comoro.