Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy atafikishwa mahakamani leo anatuhumiwa kujaribu kutoa hongo kwa jaji na kupelekea ushawishi, ikiwa ni moja ya uchunguzi kadhaa wa jinai ambao unatishia kuweka aibu kubwa katika utumishi wake wa muda mrefu wa kisiasa.
Waendesha mashtaka wanadai Sarkozy alijitolea kumpatia kazi ya fedha nyingi Jaji Gilbert Azibert huko Monaco kwa malipo ya habari ya siri juu ya uchunguzi wa madai kwamba Sarkozy alikuwa amekubali kupokea malipo haramu kutoka kwa mrithi wa L’Oreal Liliane Bettencourt kwenye kampeni yake ya urais ya mwaka 2007.
Sarkozy, ambaye aliongoza Ufaransa kutoka mwaka 2007 hadi 2012 na amebaki na ushawishi mkubwa kati ya wahafidhina, amekanusha makosa yoyote katika uchunguzi wote dhidi yake na kupambana vikali ili kesi hizo zifutwe.
Wachunguzi kutoka mwaka 2013 walikuwa wakisikiliza mazungumzo kati ya Sarkozy na wakili wake Thierry Herzog walipokuwa wakichunguza madai ya ufadhili wa Libya katika kampeni ya Sarkozy ya mwaka 2007.
Wakati wakichunguza waligundua kwamba Sarkozy na wakili wake walikuwa wakiwasiliana kwa kutumia simu za mkononi zilizosajiliwa kwa majina ya uwongo. Simu ya Sarkozy ilisajiliwa kwa jina la Paul Bismuth.