Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amewakabidhi kompyuta aina ya laptop wanafunzi wa kidato cha nne na sita waliofanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Ikulu Zanzibar.
Hafla hiyo ya kuwazawadia kompyuta aina ya Laptop wanafunzi hao imefanyika leo ukumbi wa Tibirinzi Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.
Aidha , Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali imejikita kwenye kuimarisha miundombinu kwa Skuli zote ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wengi ikiwemo kuondosha mikondo kwa skuli zote za Unguja na Pemba kwa kuendelea kujenga Skuli za ghorofa za Msingi na Sekondari ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kuhudhuria masomo ya madrasa wakati wa jioni kwa kuwa na mkondo mmoja.
Kwa upande mwingine miongoni mwa Wanafunzi waliowakilisha wenzao kupokea kompyuta hizo ni Hajra Khamis Ali, Haitham Omar Abdallah na Salum Ahmed Nassor wote kutoka Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro na Lukman Mohamed Ali kutoka Skuli ya Sekondari Chasasa, Wete Pemba.