Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane imekusudia kushughulikia suala la mishahara kwa watumishi wa umma kama ilivyo kwenye mpango wa awamu iliyopita mara tu uchumi wa nchi utapoimarika.
Rais Mwinyi ameeleza hayo leo, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi visiwani Zanzibar ambapo amesema awamu ya saba kwenye suala la mshahara ilifanikiwa katika kuanzisha awamu ya kwanza ya kima cha chini lakini mlipuko wa ugonjwa wa corona ulipelekea kushuka kwa makusanyo ya kodi na kuathiri upande wa mishahara.
“Suala la mishahara, serikali ya wamu ya saba ilikuwa na mpango mzuri kabisa wa kuongeza maslahi ya wafanyakazi kwenye mishahara kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ni kima cha chini kuwafikisha kwenye laki tatu, awamu ya pili watumishi wa kada ya kati na awamu ya tatu ni viongozi wa juu, ilifanikiwa katika kuanzisha ile awamu ya kwanza,” Rais Mwinyi
“Awamu ya nane tumeingia tukiwa na nia ileile kulitekeleza ambalo limepangwa na kwakweli hali ya uchumi ikiimarika kidogo tu, tutaanza na kada ya kati hapa ndipo walipo wataalamu mbalimbali na wanastahili kufikishwa sehemu nzuri ya mishahara,” Rais Mwinyi