Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika mjini Maputo nchini Msumbiji.
Mkutano huo umejadili ajenda mbalimbali zikiwemo zinazohusu mtangamano wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, fursa mbalimbali za kiuchumi, pamoja na changamoto za kiusalama.
Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Msumbiji Filipe Jancinto Nyusi amesema jitihada za pamoja kutoka nchi wanachama wa ukanda wa SADC zinahitajika zaidi katika kukabiliana na tatizo la ugaidi linaloikabili nchi hiyo, kwani limekuwa likirudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa Msumbiji na nchi wanachama.
Aidha, masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa dharura ni maambukizi ya Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (UVIKO 19), uanzishwaji wa kituo cha majanga, masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, biashara na Uwekezaji katika ukanda wa Jumuiya hiyo ya SADC.
Rais Nyusi amezisisitiza nchi wanachama kuendelea kuunga mkono jitihada za Taasisi za Utafiti katika kufuatilia taarifa za kusambaa kwa UVIKO 19 na mawimbi mapya ya ugonjwa huo na kuendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia maambukizi mapya.
Kuhusu changamoto za tabianchi, Mhe. Rais Nyusi amesema baadhi ya nchi wanachama zimekumbwa na uhaba wa mvua na nyingine kupata mvua nyingi zaidi na kufanya uwepo wa uwezekano kwa baadhi ya nchi kukumbwa na uhaba wa chakula.
Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maenendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umefanyika sambambana na maadhimisho ya miaka arobaini tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, ikiwa na kauli mbiu “ Kuimarisha Amani na Usalama, Kuhamasisha Maendeleo na Ustahamilivu wa Changamoto Zinazoikabili Dunia”.
Mhe. Rais Samia amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Msumbiji na kurejea Jijini Dodoma nchini Tanzania.