MPAKA jana Jumatatu jioni, straika wa Yanga, Emmanuel Okwi, alikuwa hana mawasiliano na Mwanasheria wake, Edgar Aggaba, juu ya mustakabali wa mkataba wake na klabu hiyo na kocha wake, Hans Van Der Pluijm, amemwondoa haraka katika kikosi kitakachocheza na Simba katika funga dimba ya Ligi Kuu Bara Jumamosi.
Ishu iko hivi, Pluijm wakati anaondoka na timu yake kwenda Arusha kucheza na Oljoro JKT, alimwacha Okwi Dar es Salaam ili amalizane na uongozi juu ya matatizo yake ya malipo ya sehemu ya fedha yake ya usajili, lakini hadi jana Jumatatu jioni hakuwa amemalizana nao.
Naye Aggaba alipozungumza na Mwanaspoti wikiendi iliyopita, alisema anaisubiri Yanga imalizane na mteja wake hadi juzi Jumapili jioni na kama hakuna kitakachofanyika atawasiliana na Okwi ili wavunje mkataba kila mtu aishie zake.
Si Okwi wala Yanga waliowasiliana na Aggaba, ndipo Mwanasheria huyo aliposema: “Nilikuwa nafikiria kumtafuta Okwi kujua nini tatizo lake, lakini nimejiuliza kwa nini yupo kimya mpaka sasa huku anakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kimkataba na Yanga? Nimeachana naye mpaka atakaponitafuta yeye.”
Wakati Aggaba akisema hivyo, Pluijm naye alisema: “Sitaki kuwaharibu wachezaji wengine ambao wanaweza kukosa morali kwa kulazimisha Okwi kucheza mchezo wa mwisho wakati hakuwa kambini kwa muda mrefu, ni vigumu kumpa nafasi hiyo, hilo nimeshawaeleza hata uongozi wa timu.”
Kauli hiyo ya Pluijm inamaanisha Okwi ameondolewa katika kikosi hicho na ili aichezee Yanga ni mpaka msimu ujao wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Septemba mwaka huu.
Straika huyo amejiondoa katika kikosi cha Yanga kwa kile kinachoelezwa kushinikiza alipwe sehemu ya fedha zake za usajili zilizobaki ambazo aliahidiwa kulipwa mapema mwaka huu.
Wakati huohuo, Yanga leo Jumanne inatarajiwa kucheza mchezo kirafiki mjini Moshi dhidi ya Pannone ambao ni mabingwa wa Mkoa wa Kilimanjaro msimu huu.
SOURCE: MWANASPOTI