Serikali imetoa wito kwa Wananchi wote ndani na nje ya nchi kutambua kwamba, hakuna mabadiliko yaliyofanyika kuhusu ufundishaji wa somo la Kiswahili katika Shule za Sekondari kwakuwa Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na hilo halina mabadiliko na ni lugha iliyopewa hadhi ya kutumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika pamoja na Umoja wa Afrika.
Kauli hiyo inakuja baada ya kuenea kwa taarifa kuhusu ufundishaji wa somo la Kingereza na kufungia matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye shule za Sekondari–“Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeona mijadala na taarifa mbalimbali zisizosahihi kuhusu ufundishaji wa somo la Kingereza na kufungia matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye shule za Sekondari”
“Mijadala na taarifa hizo zimewasilishwa kwa namna tofauti, jambo ambalo limesababisha mkanganyiko kwa jamii na kumekuwa na upotoshwaji ambao umesambaa ndani na nje ya nchi juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili na Kingereza kwenye Shule za Sekondari nchini”
“Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeona vyema kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa hizo kuwa Serikali katika mabadiliko ya mitaala ya mwaka 2010 na Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 hayakufanya mabadiliko kwenye lugha ya kufundishia na kujifunzia katika Shule za Sekondari”