Serikali imesema itaendelea kutoa mafunzo endelevu kwa Walimu nchini ili kuwajengea umahiri katika masomo na mafunzo wanayotoa ikiwa ni moja ya kipaumbele katika Sera ya Elimu Toleo la 2023.
Hayo yameelezwa April Mosi 2024 mkoani Morogoro na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo akifungua Mkutano wa Walimu na Watumishi wa Shule za Kanisa la Waadventista wa Sabato wa Unioni Misheni ya Kusini mwa Tanzania ambapo amesema lengo la serikali ni kutoa elimu bora na Walimu ni nyenzo muhimu kufikia lengo hilo.
“Elimu bora inahitaji walimu wenye sifa, na mwaka huu tunaanza mafunzo ya ualimu kwa wahitimu wa kidato cha Sita, lakini pia tutawahamasisha waliopo kazini wajiendeleze kupitia mafunzo endelevu ya walimu kazini’’ alisema Prof. Nombo.
Amebainisha kuwa serikali imeanza kutekeleza maboresho ya Mitaala ya elimu ngazi ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu, maboresho haya yanalenga kuandaa wahitimu wenye maarifa, mwelekeo, maadili na ujuzi unaoakisi mahitaji ya Taifa letu na kuweza kushiriki kikamilifu katika soko la ajira duniani.
“Mitaala yetu mipya itawafundisha vijana wetu masomo yote kwa umahiri na kujenga ujuzi, wakati tunatekeleza hayo ni lazima tuwafundishe kujitegemea na kusimama kama vijana walioelimika. Hivyo elimu ya kiroho itawasaidia sana kuwalinda na madhara ya utandawazi na kuwaimarisha,” amesema Nombo
Aidha Prof. Nombo amesema Wizara inathamini mchango wa muda mrefu wa Kanisa hilo katika utoaji wa elimu kwa kuzingatia viwango vya juu vya taaluma pamoja na kukuza elimu ya kiroho na kwamba Serikali itaendelea kusimamia ubora kupitia Sheria, Kanuni na Miongozo katika kuhakikisha elimu inayotolewa inawajengea watoto maarifa, maadili na ujuzi ili waweze kushiriki kwa ufanisi katika maendeleo yao binafsi, jamii na Taifa kwa ujumla.