Serikali imetoa maelekezo ya kisheria (Compliance Order) ili kuwataka waajiri kote nchini kutoa Mikataba kwa wafanyakazi madereva.
Maelekezo hayo ya serikali yametangazwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi kufuatia hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.
“Katika kushughulikia malalamiko na hoja hizo,tulikutana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva kwa lengo la kusikiliza hoja na malalamiko yao tarehe 24 Aprili, 2022, baada ya kupokea hoja hizo, Serikali iliahidi kuzifanyia kazi katika kipindi cha siku 90 na kutoa taaarifa rasmi ambayo ndiyo hii tunayoitoa kwa umma.”
Amesema ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti, 2022 Serikali itaanza kuwachukulia hatua waajiri ambao watabainika kukaidi maelekezo ya Serikali. Asema katika kuhakikisha Madareva wanapatiwa Mikataba ya Kazi, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya kaguzi zinazoshirikisha wadau wanaoguswa na sekta hii na tayari kaguzi zilifanyika katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mbeya ambapo Jumla ya Kampuni 73 zilikaguliwa na kubaini baadhi ya waajiri hawajatoa mikataba kwa Madereva.
Mhe. Katambia pia amesema kupitia kaguzi zinazoendea kufanyika katika maeneo ya kazi, Serikali itasimamia suala la Madereva kupatiwa hati za malipo ya mshahara (salary slip) kama inavyoelekezwa kwenye Sheria.
Aidha Serikali inawashauri Madereva kufanya makubaliano na waajiri wao kuhusu utaratibu gani utumike kuwalipa mishahara kwani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366 imeruhusu mwajiri na mfanyakazi kukubaliana namna ya kulipana mshahara ama kupitia benki, fedha taslim au hundi, alisema
Aidha Sheria inawataka waajiri wote kuwasajili na kuwachangia wafanyakazi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na WCF) wakiwemo wafanyakazi Madereva.
“Katika ukaguzi uliofanyika awali ilibainika kuwa baadhi ya waajiri hawajawasajili Madereva wao katika Mifuko hiyo, hivyo maelekezo ya kisheria yametolewa. Serikali itaendelea kufuatilia waajiri hao ili kuhakikisha wanatekeleza Sheria ipasavyo.” Alisema.
Mhe. Katambi amesisiitiza.suala la Bima ya Afya, kwa kuwa ni suala la makubaliano, wamiliki wapo tayari kukubaliana na Madereva kuhusu utekelezaji wake.
Aidha, ameongeza kuwa wamiliki wote wa mabasi wameelekezwa kufunga vidhibiti mwendo kwenye mabasi yao ndani ya miezi 6 hadi ifikapoa Septemba, 2022).
Masuala mengine ambayo serikali imeyachukulia hatua ni posho za mileage na overstay zilifikiwa makubaliano ambapo mileage itakuwa ni shillingi 700,000 na posho ya overstay baada ya siku 20 itakuwa ni dola 10 za kimarekani kwa siku.
Aidha, posho za returns na za kupakia na kushusha mzigo hazikufikiwa muafaka ambapo kwa upande wa madereva walihitaji returns ya shilingi 350,000 na upande wa Waajiri walifikia shillingi 300,000. Kuhusu posho ya kushusha na kupakia mzigo madereva walihitaji dola 200 za kimarekani na waajiri walifikia dola 150 za kimarekani.
Serikali imeridhia maoni ya kiwango cha malipo ya retuns kuwa shilingi 330,000 na malipo ya kushusha na kupakua mzigo kuwa dola 170 za kimarekani.
Serikali inasisitiza Madereva waendelee kujisajili kwenye Kanzi Data ya LATRA ili kukidhi matakwa ya Sheria.