Mtoto wa Rais wa zamani wa Angola Jose Eduardo dos Santos, Isabel dos Santos amekanusha madai ya ufisadi baada ya Mahakama ya Luanda nchini Angola kufunga akaunti zake za benki na kushikilia mali zake ambazo zinathamani ya Dola BILIONI 1 ambayo inatajwa kuwa nusu ya utajiri wake, Isabel mwenyewe amesema madai dhidi yake yamechochewa kisiasa
Isabel dos Santos anayeaminiwa kuwa Mwanamke Tajiri zaidi kwenye bara la Afrika anachunguzwa kwa madai ya kufanya ubadhirifu wa fedha na kuzisababishia hasara kubwa kampuni za Serikali ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya mafuta ya Taifa ‘Sonangol‘.
Baba yake ambae ni Jose Eduardo dos Santos aliitawala Angola kwa miaka 38 na utawala wake unahusishwa na kukithiri kwa ufisadi na ubaguzi kwa madai kwamba alipokua Rais, dos Santos aliwapendelea watu wa familia kwa kuwapa vyeo Serikalini hadi Rais Joao Lourenco alipochukua nafasi yake mwaka 2017.
Isabel, kama wengine wa familia ya dos Santos, aliondoka Angola kwa kudai anakabiliwa na vitisho vya kuuwawa baada ya baba yake kuondoka madarakani, unaambiwa Mwanamke huyu aliteuliwa kuwa mkuu wa kampuni ya mafuta ya taifa iitwayo Sonangol mwaka 2016 lakini alitolewa kwenye cheo hicho mwaka 2017 ikiwa ni hatua za mwanzo zilizofanywa Rais mpya wa Angola Joao Lourenco kuwaondoa jamaa za dos Santos kutoka kwenye nyadhifa mbalimbali.
Mahakama ya Angola, kama sehemu ya upelelezi wake imetoa amri ya kuzifunga akaunti za benki za Isabel dos Santos na Mumewe Sindika Dokolo ambapo taarifa zaidi zinasema kuwa hisa zao katika kampuni kadhaa za Angola ikiwemo kampuni ya simu ya Unitel na kampuni ya simenti ya Cimangola, pia zimeshikiliwa na Mahakama.
Mtoto mwingine wa Rais huyo wa zamani, Jose Filomeno dos Santos (41) ambae ni Kaka wa Isabel dos Santos, alifikishwa Mahakamani kwa tuhuma za ufisadi December 2019 akituhumiwa kufuja USD bilioni 1.5 kutoka kwenye mfuko wa mali za taifa la Angola wakati wa alipokuwa Mkuu wa mfuko huo kuanzia mwaka 2013 hadi 2018.
Uamuzi wa mahakama hiyo pia unamuhusu Mfanyabiashara wa Ureno, Mario da Silva, Familia yake inailaumu Serikali ya Rais Lourenco kwa misukosuko inayomkabili da Silva.
Darias Jonker Mkurugenzi wa bara la Afrika wa Eurasia Group, kampuni ya ushauri inayohusika pia na utafiti wa masuala ya kisiasa amesema kufungiwa mali za familia ya dos Santos inaonyesha kwamba Rais wa sasa Joao Lourenco anahisi sasa anaweza kusonga mbele dhidi ya familia ya dos Santos katika vita dhidi ya ufisadi bila kuhatarisha ushawishi wake ndani ya chama tawala cha MPLA.
kwa mujibu wa DW Kiswahili, licha ya utajiri mkubwa wa mafuta, gesi na madini, Wananchi wengi wa Angola wanaishi katika umaskini na wanaendelea kutegemea kilimo kwenye mashamba madogomadogo kujikimu mahitaji yao ya msingi.
VIDEO: MTANZANIA ANAELIPWA MAMILIONI KWA KUCHOMA MAITI ZA WACHINA
VIDEO: RAIS MAGUFULI AKIENDESHA BOTI, MKEWE AKIVUA SAMAKI