Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa maarufu kama Mafisadi imesema kwamba mfanyabiashara Abdu Nsembo (45) na mke wake Shamimu Mwasha (41), wana kesi ya kujibu.
Mahakama hiyo imesema wanafamilia hao wataanza kujitetea kesho yaani Septemba 3.
Uamuzi huo umetolewa na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Elinaza Luvanda baada ya kusikiliza mashahidi wanane na vielelezo sita vya Jamhuri.
Hata hivyo, washtakiwa waliieleza mahakama kwamba wanatarajia kuita shahidi mmoja pamoja na wenyewe, utetezi utakuwa na mashahidi watatu.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronica Matikila na Wakili wa Serikali Constantine Kakula.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha dawa hizo za kulevya, Mei Mosi, mwaka huu, wakiwa eneo la Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini DSM kinyume na sheria ya uhujumu uchumi.