Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu leo Juni 3, 2024 akiwa katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam, amefanya kikao na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, Vyuo Vikuu, washirika wa Maendeleo, makampuni ya Bima binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na kujadili masuala yanayohusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote Na. 13 ya mwaka 2023.
Kikao hicho kimeangazia namna bora ya kuongeza wanachama katika skimu za bima ya afya na kuhakikisha skimu za bima ya afya zinaendelea kuwa himilivu katika kutoa huduma kwa wanachama na wanufaika.
Awali akifungua kikao hicho Dkt. Jingu amesema malengo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inaweka mazingira rafiki ya kuwezesha kila mtanzania anakuwa na uhakika wa kupata huduma bora za afya kupitia utaratibu wa bima ya afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ambaye ni mmoja wa washiriki wa kikao hicho amesema Serikali imeimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuongeza idadi ya vituo na usimikaji wa vifaa na vifaa tiba katika vituo. Changamoto iliyopo sasa ni wananchi kupata huduma za afya pasipo kuingia katika janga la umaskini ambapo hilo linawezekana kwa kuhakikisha wananchi wanajiunga na utaratibu wa bima ya afya.
Wadau kwa ujumla wao wameshauri kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi ili kufahamu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya, Kuboresha ubora wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na huduma kwa mteja hali itakayochochea umuhimu wa wananchi kujiunga pasipo kulazimishwa pamoja na kuweka mifumo rahisi ya usajili wa wananchi hususan katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kutumia mawakala, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na makampuni ya simu.