Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema zinahitajika nguvu za pamoja kutoka kwa viongozi wote wa serikali duniani na kwa haraka sana ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoikabili dunia baada ya ripoti mpya ya wanasayansi kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC iliyotolewa leo kubainisha kuwa shughuli za binadamu zinapeleka dunia katika madhara ya tabianchi yasiyorekebishika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo mjini New York, Marekani kuhusu uchambuzi wa ripoti hiyo, Guterres amesema, ripoti imeonesha shughuli za kibinadamu zinazidi kuiathiri sayari dunia na joto limezidi kuongezeka ilihali kuna makubaliano yaliyofanyika Paris ya nchi zote kupunguza gesi ya ukaa.
“Ripoti ya leo ya IPCC imeonesha alama ya hatari, shughuli za kibinadamu zinaendelea kuathiri dunia na haziwezi kukanushwa kwani kuna ongezeko la uzalishaji wa gesi ya ukaa, ukataji wa miti na shughuli zote hizi zinawaweka mabilioni ya watu katika hatari. Joto limeathiri kila kona ya dunia na mabadiliko mengi hayatabiriki.”