Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi amezipongeza wizara zote mbili husika kwa maandalizi mazuri ya maadhimisho hayo ambayo yanahitimishwa leo tarehe: 7 Julai 2023.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kupewa heshima ya kuwa na siku yake maalum ya maadhimisho.
Sambamba na hayo Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Bakiza na Bakita katika kukiendeleza Kiswahili ikiwa pamoja na kusambaza kamusi na vitabu katika balozi mbalimbali kwa kutoa taaluma na kufundishia.
Rais Dk. Mwinyi pia, amezipongeza Balozi zetu za Tanzania nje ya nchi ikiwemo Korea ya Kusini, Italia, Falme za Kiarabu, Uholanzi, Zimbabwe, Ufaransa, Cuba, Nigeria na Sudan ambazo zimefungua vituo vya kufundishia Kiswahili.