Klabu ya Simba imesaini mkataba wa miaka minne na Kampuni ya uuzaji na ukodishaji magari ya Africarriers kwa ajili ya kuzisafirisha timu ikiwamo ya wakubwa, Wanawake (Simba Queens) na vijana chini ya umri wa miaka 17 wenye thamani ya Sh milioni 800.
Africarriers wametoa basi kubwa aina ya Golden Dragon la kisasa lenye uwezo wa kubeba abiria 60 kwa timu ya wakubwa, Eicher yenye uwezo wa kubeba watu 35 kwa ajili ya Timu ya Wanawake na Costa kwa ajili ya Timu ya Vijana.
Kwa mkataba huo, Africarriers wanakuwa wasafirishaji rasmi wa timu ya Simba tatu kwa njia ya barabara kama ilivyo kwa Air Tanzania kwa njia ya anga.
Mkurugenzi wa Masoko wa Africarriers, Zain Pirbhai amesema kama moto wao unavyosema ‘We Drive Africa’ na Simba wanafanya vizuri kwenye michuano ya Afrika hivyo wanafurahia kufanya kazi nao.
“Itakuwa faida kwa pande zote mbili katika mkataba huo na anaamini katika miaka minne hii kila kitu kitakwenda sawa,” amesema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez amesema jezi za timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 itakuwa na nembo ya Africarriers kifuani wakati zile za kusafiria za wakubwa na zile za Simba Queens zitakuwa na nembo hiyo mkononi.
“Kwa muda wa miezi minne walikuwa wanaisafirisha timu yetu ya Wanawake ya Simba Queens na wameona faida waliyopata kufanya kazi na Simba wameamua kuingia mkataba huu kwa timu zote nasi tunashukuru kwa hilo,” Barbara.