MTANZANIA
Mtu aliyesadikiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza amezikwa kwa tahadhari kubwa na wataalam wa afya.
Wakati mtu huyo akizikwa jana hofu kubwa imetanda Mikoa ya kanda ya ziwa huku watu wakiogopa kugusana katika vyombo vya usafiri na kutumiana ujumbe mfupi wa simu za mkononi juu ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.
Mgonjwa aliyefariki alitajwa kwa jina la Salome Richard (17) ambaye ndugu zake walizuiwa kumwona na kutoa heshima za mwisho makaburini huku akizikwa kwa uangalizi maalum.
Mganga Mkuu Hospitali ya Sengerema Mary Jose alisema mwili wake umezikwa na wataalam wa afya ikiwa ni hatua za kuchukua tahadhari na kukana kuwa hakuna ugonjwa wa Ebola bali wamechukua tahadhari tu kwani mgonjwa huyo alikua na dalili kama za ugonjwa wa Ebola.
MTANZANIA
Waumini wa kanisa la Anglikana Wilaya ya Nyamagana Mwanza walisimamisha kwa muda shughuli za ibada kanisani hapo baada ya kutokea vurugu kubwa.
Vurugu hizo zilitokea baada ya baadhi ya waumini hao kumtuhumu Askofu wa kanisa hilo Boniface Kwangu kwamba ni mmoja wa wafuasi wa kundi la Freemasons na hufanya kazi za kundi hilo.
Mmoja wa waumini wa kanisa hilo Shadrack Lazaro alitoa tamko la jinsi askofu wao anavyofanya kazi na kundi la Freemason ndipo waumini walipomvamia na kumtoa nje ya kanisa kwa nguvu na kusababisha vurugu kubwa.
Muumini huyo alisema pamoja na sababu kadhaa za kumkataa askofu huyo pia hawaridhishwi na tabia yake ikiwemo kutaka kubomoa sakafu akidai kuna irizi imefichwa na baadhi ya waumini wake kanisani hapo.
MWANANCHI
Familia ya watu watatu Wilayani Nzega Tabora ya Leticia Thomasi na watoto wake wawili wameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Leticia aliuawa pamoja na watoto wake Marietha Thomas wa darasa la pili na Margret Thomas wa darasa la kwanza wote wa shule ya Msingi Mwamalulu usiku wa kuamkia jana huku sababu ikitajwa ni wivu wa mapenzi lakini wahusika bado hawajafahamika.
Kamanda wa Polisi Tabora amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha watuhumiwa kupatikana na kuwataka kutojichukulia sheria mikononi kwani husababisha madhara makubwa kwa jamii.
MWANANCHI
Maharusi Lameck Yesse na Gladmarry Mushi wa Wilayani Rombo wameacha gumzo baada ya kukodi Helkopta kutoka Kenya kunogesha harusi yao na kuruka nayo angani.
Tukio hilo lilitokea juzi alasiri katika mji mdogo wa Tarakea uliopo mpakani mwa Tanzania na Kenya na kuvuta hisia za watu wengi baada ya tukio hilo kuwa la kwanza kutokea mjini hapo.
Maharusi hao walifunga harusi katika kanisa la KKKT usharika wa Tarakea na ibada iliongozwa na mchungaji Emmanuel Dedeok.
MWANANCHI
Maaskofu wa kanisa katoliki wamekataa kutambua haki za wapenzi wa jinsia moja katika mkutano wao mkuu wa Synod uliomalizika juzi.
Hoja kuu zilizotawala mkutano huo ni iwapo wapenzi wa jinsia moja wanaweza kutambuliwa na kanisa hilo au la,na iwapo wanandoa wanaoishi pamoja bila kubariki ndoa na wale waliooana na kuachika wanaweza kupatiwa sakramenti.
Kura hiyo ilipigwa juzi baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa wiki mbili ilishindwa kufikia theluthi mbili baada ya kuibuka mvutano mkali katika mkutano huo licha ya Papa Fransis kuwataka kuliangalia suala hilo katika misingi ya huruma.
NIPASHE
Mtoto aliyeibiwa Dodoma akiwa na siku nane baada ya mama yake Teddy Bishaliza kunywesha juisi inayosadikiwa kuwekwa dawa za kulevya amepatikana akiwa hai chini ya Mti.
Mtoto huyo aliibiwa usiku wa kuamkia Alhamis iliyopita na kupatikana ijumaa huku kitovu chake kikiwa kimetoka na kuonekana akiwa tofauti na kabla hajaibiwa.
Bibi wa mtoto huyo Jane Pius ambaye ndiye alilisaidia Jeshi la Polisi kumtambua mtoto huyo alisema alifuatwa na askari hao hospitali wakati akimuuguza mwanaye ambaye bado alikua hajawa katika hali ya kawaida kutokana na juisi aliyokunywa na kuongozana nao hadi alipo mtoto huyo na kumtambua huku akiwa tofauti kabisa.
Anasema alikutwa na nguo ambazo hakuwa nazo mara ya mwisho huku akiwa amepakwa wanja kwenye nyusi uliochorwa alama ya nyota na mwezi kwenye paji la uso pamoja na masikio yake kuondolewa uzi ambao aliwekewa na mama yake mzazi baada ya kutobolewa masikio tofauti na alivyokua awali.
NIPASHE
Mtoto Hassan Masasi mwenye miaka saba wa darasa la aliyetoroka nyumbani kwao Moshi ameonekana Jijini Dar es salaam.
Mtoto huyo alisema wakati anaondoka nyumbani kwao hakugombezwa na mtu wala kufanyiwa kitendo chochote kibaya isipokua aliamua mwenyewe kupanda basi bila kulipa nauli lakini hakujua anakwenda wapi.
Alipofika Dar alipanda magari mawili na kujikuta yupo kituo cha Bom bom na kusaidiwa na msamaria mmoja ambae hamfahamu na baadaye kumpa chakula kisha kumpeleka kituo cha Polisi Mwenge huku akisema yupo tayari kurudi nyumbani kwao Moshi.
TanzaniaDAIMA
Wanafunzi wawili wa darasa la pili wenye miaka saba na mwingine nane wa Shule ya Msingi Kikunku Kigoma wameadhibiwa na walimu wao kutokana na tabia yao ya kufanya mapenzi katika umri mdogo na kusababisha walimu watatu kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumjeruhi mtoto wa kiume.
Akizungumzia tukio hilo mwalimu mmoja wa shule hiyo Nicholous Ulimwengu alisema wazazi wa watoto hao walilamika wanafunzi hao kila siku kuchelewa kurudi nyumbani na kuamua kufuatilia shuleni hali iliyowafanya walimu kuchunguza na kugundua huwa mara baada ya masomo kuenda sehemu ya kujificha na kufanya tendo hilo.
Alisema baada ya kugundua tabia za wanafunzi hao walimu waliamua kuwaadhibu kwa kuwachapa viboko vinne kila mmoja ambapo mzazi wa mtoto wa kiume aliamua kwenda kushtaki polisi baada ya mwanae kulalamika kupata majeraha ndipo polisi wakaamua kuwashikilia walimua hao kutokana na adhabu hiyo wakati uchunguzi ukiendelea.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook