Leo September 27,2018 Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hadi sasa hajapata wakili wa kumtetea katika kesi ya uchochezi inayomkabili yeye na viongozi 8 wa CHADEMA.
Msigwa ameyaeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde amedai kuwa hadi sasa bado hajapata wakili hivyo anaiomba mahakama impe muda ili aweze kupata wakili.
Msigwa ameyaeleza hayo baada ya Wakili wa Serikali, Simon Wankyo kubainisha kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa Maelezo ya awali (PH) na kwamba Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri anayeisikiliza kesi hiyo yupo likizo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde ameahirisha kesi hiyo hadi October 25, 2018 ili kumpa muda wa kutosha Msigwa kutafuta wakili wa kumtetea.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo, ambao wanatetewa na wakili Peter Kibatala ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.
Msigwa anatafuta wakili wa kumtetea baada ya wakili Jeremiah Mtobesya aliyekuwa akimtetea kujitoa kumtetea katika kesi hiyo.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.