Mshambuliaji, Amissi Tambwe, wa Simba amefikisha mabao 19 katika Ligi Kuu Bara baada ya jana Jumapili kuiwezesha timu yake kushinda mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting.
Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Taifa, Tambwe ambaye ni raia wa Burundi, aliifungia Simba mara mbili dakika za 23 na 33.
Bao la kwanza alilifunga akimalizia mpira uliotemwa na kipa Abdallah Rashid wakati akiokoa shuti kali la Said Ndemla. La pili alilifunga pale alipounganisha krosi safi ya Haroun Chanongo.
Mabao hayo yanamfanya Tambwe kuvuka rekodi ya Boniface Ambani aliyefunga mabao 18 msimu wa 2010/11 alipokuwa Mfungaji Bora.
Bao la tatu la Simba katika mchezo huo uliohudhuriwa na watazamaji wachache huku mvua ikitawala muda mwingi, lilifungwa na Chanongo dakika ya 75 baada ya kupokea pasi ya Amri Kiemba.
Ruvu Shooting ilipata bao la kwanza dakika ya 68 lililofungwa na Said Dilunga kwa kichwa akiunganisha kona ya Michael Aidan. Bao la pili la Ruvu lilifungwa kwa njia ya penalti dakika ya 82 na Jerome Lembele.
Mwamuzi, Nathan Lazaro, wa Kilimanjaro alitoa penalti hiyo baada ya beki wa Simba, Joseph Owino, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Licha ya ushindi huo, Simba imebaki katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 35 kwani Mbeya City ina pointi 36 katika nafasi ya tatu baada ya juzi Jumamosi kutoka suluhu na Oljoro JKT.