Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro ametoa tahadhari kwa Wakazi wa Ruvuma kuwa tembo zaidi ya 200 wapo nje ya Hifadhi Taifa ya Mwl.Nyerere kutokana na Wafugaji kuingiza makundi ya ng’ombe ndani ya Hifadhi hiyo.
Dkt. Ndumbaro ametoa tahadhali hiyo hususania kwa wakazi wa wilaya Tunduru na Namtumbo wakati alipotembelea vijiji sita vilivyoathiriwa zaidi na tembo ili kukutana na wananchi na kujibu kero mbalimbali zinazotokana na uvamizi wa tembo katika maeneo yao wakitokea Hifadhi ya Taifa ya Mwl.Nyerere.
Amesema Wenyeviti wa Vijiji wamekuwa wakiwakaribisha Wafugaji kutoka katika mikoa mbalimbali kuhamia katika maeneo ya vijiji hivyo na makundi makubwa ya ng’ombe na kisha kuingiza mifugo hayo ndani ya Hifadhi kwa ajili ya kupata malisho.Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Satelite uliofanyika hivi karibuni umeonesha tembo zaidi 200 wapo nje ya Hifadhi, Hivyo amewatahadharisha wananchi kutoa taarifa haraka pindi wanapoona makundi ya tembo yakiwa karibu kwenye makazi yao.
Amesema kufuatia ng’ombe hao kuingia ndani ya Hifadhi wamekuwa wakilazimika kutoka nje ya maeneo yao kwa sababu tembo hawapendi kuchangamana na ng’ombe kutokana na harufu ya madawa wanayotumia kuoshewa wakiwa katika majosho.Kutokana na hali hiyo, Waziri Dkt.Ndumbaro ameagiza ng’ombe walioingizwa ndani ya Hifadhi hiyo wafugaji walipe faini na ng’ombe hao wataifishwe na wasipouzika wapewe magereza kwa ajili ya chakula cha Wafungwa.
Aidha, Waziri Ndumbaro ametaja sababu nyingine iliyochangia Tembo kutoka nje ya Hifadhi kuwa ni tabia ya baadhi ya Wananchi kulima kwenye kingo za Hifadhi hali inayowavutia tembo kutoka nje kwa ajili ya kula mazao hayo.Amesema idadi ya mashamba pamoja na wananchi kujeruhiwa inazidi kuongezeka siku hadi siku si kwa sababu idadi ya tembo imeongezeka bali ni kutokana na idadi ya watu kuongezeka na kulazimika kufanya shughuli ndani ya Hifadhi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amewaonya Wananchi kuacha kulima katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Wananchi kuwa hali hiyo imechangia tembo kutoka nje ya Hifadhi kula mazao.
Awali akieleza kuhusu kero za wananchi wa jimbo lake la Namtumbo Mhe. Vita Kawawa, amesema kuwa wananchi wa Jimbo lake la Namtumbo kwa muda mrefu sasa wamekuaa wakiathiriwa na tembo wanaovamia makazi na mashamba yao na kumuomba Waziri wa Maliasili na Utalii kuharakisha kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa Wananchi waliopata adha zitokanazo na adha ya tembo.
Kwa upande wa Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Hassan Kungu amemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ndumbaro kuongeza fedha za vifuta jasho na vifuta machozi kwa sababu fedha wanayolipwa wananchi wake hailingani na thaman ya mashamba waliyoharibiwa na tembo.
MDOGO WA JIMMSON ASIMULIA AIBUKA MAPYA MAJAMBAZI WALIVYOMVAMIA KAKA YAKE, “DAMU ILIMUISHIA”