Mhasibu Mkuu wa (TAKUKURU), Godfrey Gugai anayedaiwa kumiliki mali za Shilingi Bilioni 3 zisizoendana na kipato chake amekana makosa hayo wakati aliposomewa maelezo ya awali.
Mbali ya Gugai washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.
Katika maelezo hayo ya awali waliyosomewa na Wakili wa serikali, Awamu Mbagwa washtakiwa walikana maelezo yote ya makosa yao isipokuwa walikubali wafisu wao ikiwemo Majina, Dini, Kazi na Umri kwamba ni sahihi.
Miongoni mwa maelezo aliyoyakana Gugai ni kwamba kupitia mishahara yake na malupulupu mengine alijipatia kipato cha Shilingi Milioni 852 kutoka kwa mwajiri wake.
Pia mikopo yote aliyoipata katika benki ya CRDB, NBC, benki ya Posta na saccos ya TAKUKURU inathamani ya Sh 137 milioni.
Pia mwaka 2015/2016 kwamba alijipatia utajiri wa juu zaidi ya kipato chake halali wa Sh. Bil 3. 6
Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka June 28, 2018.
Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.
Gugai na wenzake wanasota mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.