Mkurugenzi wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Buji Bampebuye ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Ushirika kutoa maoni yatakayotumika katika kuboresha na kupitia upya Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002.
Wito huo umetolewa wakati wa ukusanyaji wa maoni hayo katika kikao kazi kilichofanyika DSM hivi karibuni, Tume ilipokutana na Viongozi wa Vyama vya Ushirika pamoja na wanaushirika waliokuwa wakijadili masuala mbalimbali ya namna bora ya kuboresha utendaji na uendeshaji wa Sekta ya Ushirika nchini.
“Wanaushirika tujadiliane kwa kina changamoto zilizopo katika Sekta tutoe mapendekezo nini kifanyike na namna gani kifanyike ili kuimarisha na kuondokana na changamoto pamoja na vikwazo vilivyopo katika Sekta ya Ushirika inayochangia Uchumi wa nchi na kutoa fursa za ajira nchini. Ushirika ni wa wanaushirika wenyewe kwa hiyo tumieni fursa hizi vizuri kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa Taifa letu,” Bampebuye
Sambamba na kikao kazi hicho Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara Juma Mokili akifungua kikao cha wadau katika ukusanyaji wa maoni mkoani Mtwara amesema Sera inatoa Dira ya uendeshaji wa Sekta ya Ushirika.
Hivyo, wadau wana mchango muhimu katika kuujenga Ushirika watumie fursa hiyo kutoa maoni yao kwa uwazi na uhuru ili kuweka msingi wa Sera bora itakayotumika kuendelea kuunda Sheria, Miongozo pamoja na Kanuni zitakazotumika kwa maslahi ya wanaushirika na Taifa kwa ujumla.
Pamoja na mambo mambo mengine wadau walijadili masuala mbalimbali ikiwemo muundo wa Ushirika, fedha, Uwekezaji katika Vyama, Usimamizi na Uendeshaji wa miradi ya Pamoja, mali za Ushirika, ubunifu na Ujasiriamali katika Ushirika, masoko ya bidhaa, huduma za Ushirika, utawala, usimamizi, utafiti, elimu pamoja na mafunzo ya Ushirika.
Kwa upande wake Mjumbe wa kikao kazi Mkoani Mtwara Issa Mangochi kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara (MAMCU) amepongeza utaratibu huo shirikishi ambao umetoa fursa kwa wadau kutoa maoni na mapendekezo yao yatakayosaidia kutengeneza Sera bora zaidi itakayo hudumia wanaushirika wengi zaidi na utendaji wenye tija na maendeleo kwa wananchi.
Aliongeza kwa kuwaomba watendaji katika Sekta ya Ushirika kufanya kazi zao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia taratibu za kazi.
Vikao kazi hivyo vimehusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vyama vya Msingi (AMCOS), Vyama vikuu, Taasisi za Vyuo vikuu, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO).
Tume tayari imeshapokea maoni kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Kilimanjaro, Kanda ya Juu Kusini mkoani Mbeya pamoja na Kanda ya Ziwa mkoani Mwanza.