Leo August 22, 2019 Hatimaye Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wamesaini makubaliano ya amani na kumaliza tofauti zao.
Idhaa ya Kiswahili ya DW iliripoti kuwa makubaliano hayo yalitiwa saini katika Mji Mkuu wa Luanda, Angola lengo ikiwa ni kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo jirani.
Kwa mujibu wa DW, makubaliano hayo yaliwekwa katika mkutano wa pili mbele ya Marais, Felix Tshisekedi (Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo), João Lourenço, (Angola) na Denis Sassou-Nguesso (Congo Brazaville) ambao walikuwa wapatanishi katika mgogoro huo.
Taarifa ya Ikulu ya Angola ilisema kuwa makubaliano hayo yamefikiwa kutokana na jitihada za nchi hiyo kwa usaidizi wa DRC.
“Viongozi hao wawili wamekubaliana kutatua mzozo wowote baina ya mataifa yao kwa njia ya amani,” liliripoti Shirika la habari la nchini Angola (Angop).
Akizungumza mara baada ya mkaubaliano hayo Rais Kagame alisema “tumekubalina kushughulikia matatizo yote ili kudumisha amani baina ya nchi zetu,”
Rwanda na Uganda kwa muda mrefu zimekuwa katika mgogoro wa kisiasa na kuathiri maisha ya watu wake kijamii na kiuchumi.