Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Saimon Sirro amesema hali ya usalama nchini kwa sasa ipo vizuri tofauti na ilivyokuwa takribani miezi miwili iliyopita.
Akizungumza katika ziara yake iliyowakutanisha Watendaji, Wenyeviti wa Mitaa pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi mkoani Arusha, amebainisha kuwa matukio ya ujambazi yalianza kushika kasi kutokana na baadhi ya watu kukata rufaa na kurejea uraiani lakini kwa sasa yamedhibitiwa.
Amebainisha kuwa matukio mengi hufanyika kwenye Mitaa ikiwemo watu kuvuta bangi, kutumia dawa za kulevya na kwamba njia pekee ya kuwakamata ni ulinzi shirikishi.
Mkuu huyo wa jeshi la polisi amewaagiza wakuu wa polisi wa wilaya kufanya vikao na wenyeviti wa mitaa na watendaji kutathmini hali ya ulinzi na usalama ili kubaini changamoto na kuziundia mikakati ya kuzimaliza.