Takribani mwezi mmoja tangu nchi ya Nepal ilipopata maafa ya tetemeko la ardhi lilochukua maisha ya maelfu ya watu – mastaa mbalimbali ulimwenguni wamekuwa wakihamasisha watu kuchangia watu waliopata madhara kwenye nchi hiyo.
Mmoja wa mastaa ambaye jina lake lilijitokeza sana ni mwanasoka bora wa dunia Cristiano Ronaldo, ambaye alitumia mitandao mbalimbali ya kijamii kuhamasisha wafuasi wake kuchangia watu waliokubwa na maafa hayo kupitia taasisi ya ‘Save the Children’ .
Pamoja na uhamasishaji lakini mapema wiki iliyopita zilisambaa taarifa kwamba Ronaldo alitoa msaada wa paundi millioni 5 kuchangia waathirika wa maafa hayo, mchezaji huyo amekuwa na tabia ya kutoa misaada mbalimbali kwa miaka kadhaa sasa.
Lakini jana kupitia taarifa rasmi ya Taasisi ya ‘Save the Children’ imefahamika kwamba hakukuwa na ukweli kuhusu Ronaldo kutoa kiasi hicho cha fedha.
Taarifa ya taasisi hiyo ilisomeka: “Balozi wa dunia wa Save the Children, Cristiano Ronaldo, ametumia sauti yake kuhamasisha watu kuwajali watoto wanaopatwa na matatizo ulimwenguni.
“Lakini taarifa za hivi karibuni kuhusu na mchango wa Ronaldo kupitia ‘Save the Children’ kwa ajili ya kusaidia watoto walioathirika na tetemeko ardhi nchini Nepal sio za kweli.
“Hata hivyo tungependa kumshukuru Cristiano Ronaldo na watu wengine mashuhuri kwa sapoti yao ya kuhamasisha michango kwa ajili ya watoto na familia zilizoathirika na tetemeko la ardhi huko Nepal.”
Inakadiriwa watu zaidi ya 8,000 wamepoteza maisha kwenye tetemeko la ardhi lilotokea mnamo April 25, kabla ya jingine lilotokea wiki iliyopita, kuua watu 16 zaidi.