Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema maboresho na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya hali ya hewa umechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa usahihi wa utabiri na kufikia wastani wa asilimia 88.3 hivyo kuchangia azma ya Serikali ya kujenga na kukuza uchumi shindani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo , Dk Agnes Kijazi amesema hayo Novemba 29, 2021 mjini Morogoro katika hotuba ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo , Dk Buruhani Nyenzi kufungua mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Mamlaka hiyo ambalo ni pili kufanyika katika kipindi cha mwaka huu (2021).
Dk Kijazi amesema, Serikali kupita Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imekuwa ikiyatekeleza maboresho na uwezeshaji huo hasa eneo la kuiwezesha Mamlaka kuwa na vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa.
Amesema , mkutano huo wa siku mbili umelenga kufanya tathimini ya utendaji wa mamkala itayosaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
“ Mnakumbua karibuni tumeshuhudia athari mbalimbali zitokanazo na mabadiliko yah ai ya hewa na tabianchi ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi vya ongezeko la joto hadi kufikia nyuzi joto 35.6 kwa maeneo ya ukanda wa Pwani,” Dk Kijazi.
Dk Kijazi ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka hiyo kila mara ili kupunguza madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa.