Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Njombe Scolastica Kevela amemkabidhi Tuzo Maalumu Rais Samia Suluhu Hassan kama zawadi kutokana na utendaji wake mzuri unaoliletea Taifa mafanikio mbalimbali.
Kevela ametoa tuzo hiyo iliyopokelewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Gaudensia Kabaka wakati wa ziara yake Mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine alikabidhiwa tuzo hiyo aliyoitoa kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo amfikishie Rais Samia.
“Tuzo hii ni ishara kuwa wananchi na zaidi sisi wanawake wa Mkoa wa Njombe tunathamini na kutambua mchango mkubwa anaoutoa Raise Samia katika kuliongoza Taifa hili, naomba mfikishie salamu zetu na tutazidi kumuombea kwa Mungu” amesema Kevela
Pamoja na tuzo hiyo kwa Rais Samia, Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huyo alikabidhi zawadi mbalimbali kwa ajili ya wajumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho iliyotolewa na UWT Wilaya ya Njombe kama sehemu ya kutambua mchango wanaoutoa kwa chama hicho kwa ‘uchapaji kazi’ wao
Awali kabla ya kuikabidhi zawadi hiyo Kevela amesema Jumuiya hiyo ya UWT Mkoa wa Njombe ipo imara na zaidi inaendelea kutekeleza majukumu yake na kuhakikisha Jumuiya hiyo na Chama kwa ujumla vinasonga mbele.
“Jumuiya yetu kuna utulivu wa kutosha na ukiona utulivu huu ujue kuna mwenyewe, niwahakikishie kuwa ndani ya jumuiya yetu tunapendana na kushirikiana tukiongozwa na jemedari wetu mkuu Mama Samia Suluhu Hassan” amesisitiza Kevela
Aidha akiwahutubia wajumbe wa Jumuiya hiyo, wanachama wa Chama cha Mapinduzi(CCM) na wananchi wakati wa ziara yake hiyo ya kikazi, Mwenyekiti wa UWT Taifa Gaudensia Kabaka amewataka wana Jumuiya hiyo kuwa kitu kimoja na kuacha mitafaruku isiyo na tija hususani kipindi hiki ambacho chama hicho kinajiandaa kufanya chaguzi zake za ndani.
“Tunajiandaa na uchaguzi, rai yangu ni kwamba mara baada ya uchaguzi kupita tuendelee kubakia kuwa kitu kimoja na zaidi tujijenge na kuwa jeshi kubwa ili tunajiandaa kwenda uchaguzi mkuu was Mwaka 2025 tuwe na jeshi kubwa ndani ya UWT” aliongeza Kabaka
Aidha aliipongeza Jumuiya hiyo Mkoa wa Njombe kwa umoja wao pamoja na juhudi mbalimbali wanazozichukua kujenga uhai wa chama hicho hasa kupitia vikao mbalimbali vya chama na kunadi sera nzuri kwa wananchi wa Mkoa huo.