Rais John Magufuli leo February 1, 2018 katika Maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Mahakama amesema yupo tayari kufanya uteuzi wa majaji wengine ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa wa majaji ambayo inasababisha mrundikano wa mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Tofauti na hilo Rais Magufuli ametoa wito kwa Mahakama kuendelea kurekebisha dosari ambazo zimekuwa zikiuchafua mhimili huo wa Dola ikiwemo Majaji na Mahakimu kujihusisha na vitendo vya upokeaji wa rushwa na ucheleweshaji wa kesi ambavyo vinasababisha hasara kubwa kwa taifa.
Aidha amempongeza Jaji Mkuu Prof Ibrahim Juma kwa hatua ya kuwafukuza kazi watumishi 112 wa Mahakama wakiwemo Mahakimu 17 waliojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili
Rais Magufuli pia ameeleza kushangazwa na vyombo vingine ambavyo hushirikiana na Mahakama kama vile Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Magereza na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kutowawajibisha watumishi wake wanaokiuka maadili.
“Mwaka jana nililalamika, sasa mwaka huu sitalalamika, nitachukua hatua, tena mwezi huu wa pili hautaisha, pale ofisini kwangu napokea barua nyingi za malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi, kila kesi upelelezi haujakamilika, ni lazima kuwe na utatuzi wa jambo hili” – Rais Magufuli
“Hivi sasa kuna kesi za Shilingi Bilioni 169.1 na Dola za Marekani Milioni 38.2 zinasubiri tu na nchi inakosa mapato” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.” – Rais Magufuli
Majibu ya Serikali Bungeni kuhusu wanaume wanaotelekeza watoto