Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kukodi gari kwa Tsh. Laki 8 pale wagonjwa wao wanapopata rufaa.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumanne, September 17, 2019 wakati akizungumza na Wananchi wa Mji wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kituo cha mabasi cha mji huo ambapo amesema iwapo fedha za makusanyo ya mapato ya ndani katika Halmashauri husika zingekuwa zinatumika vizuri kusingekuwa na changamoto kama hizo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia Wananchi wa Mji wa Ifakara kuiomba Serikali iwasaidie kuwapatia gari la wagonjwa kwani kitua chao hakina gari na wagonjwa wao wanapopata rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro wanalazimika kukodi gari kutoka hospitali ya Mtakatifu Francis kwa gharama ya Tsh. 800,000 ambazo baadhi yao wanashindwa kuzimudu.