Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua kituo cha huduma za simu kwa wateja ambacho kazi kubwa ni kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwamo magonjwa milipuko.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Ummy Mwalimu amesema kituo hicho kina uwezo wa kupokea simu 1000 kwa wakati mmoja na kuunganisha vituo vitano kwa wakati mmoja.
Amesema kazi ya kituo hicho ni kupokea maoni, taarifa, maswali na ushauri kuhusu masuala mabalimbali yanayohusu sekta ya afya na amewataka wananchi kupiga simu 199 ili wapate huduma na walioko nje ya nchi wanapaswa kupiga namba 0800110124.
Amewataka wananchi watakaopiga simu kuwa wastaarabu, kutumia lugha ya staha na kutoa taarifa sahihi ambazo zitasaidia Serikali na Wizara ya Afya kuchukua hatua stahiki na kwa wakati. Amefafanua kwamba kituo hicho kitatumika kutoa elimu na miongozo mbalimbali kuhusu masuala ya afya na kitakuwa na watalaamu 150 wakiwamo wataalamu wa afya, wauguzi na madaktari.