Kamishna wa Uhamiaji amesema kuwa raia wa Afrika Kusini Menelaos Tsampos anayekabiliwa na kesi ya kutishia kwa njia ya mtandao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hana uhalali wa kuishi nchini.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Katuga alidai licha ya kesi hiyo kutajwa, lakini wamefika na taarifa kuhusu makazi ya mshtakiwa ambapo ni kweli anaishi Dar es Salaam na ndugu zake, nyumba namba 25, Block J, ambapo wamethibitisha hilo kupitia Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.
Alidai kuwa baada ya kuthibitisha hilo kama walivyoamriwa na Mahakama, pia walimwandikia barua Kamishna Mkuu wa Uhamiaji August 15, 2017 ili kujua uhalali wa mshtakiwa kuishi nchini.
Katuga amedai Kamishna aliwajibu kupitia barua kwamba mshtakiwa huyo hatakiwi kuwepo nchini kwa kuwa hana uhalali kisheria.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Jebrah Kambole amedai kuwa barua ya Kamishna haielezi sababu za kisheria zinazomfanya mshtakiwa huyo akose uhalali wa kuishi nchini huku akisema suala la dhamana ya mshtakiwa hailingiliani na uhalali wa kuishi kwake nchini.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mkeha ameahirisha kesi hiyo hadi August 18, 2017 kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa manne ikiwemo June 22/2017 maeneo ya DSM kupitia mfumo wa Kompyuta alituma ujumbe wa E-mail uliokuwa na maneno ya vitisho kwa mtu anayeitwa Costa Gianna, ikiwa ni kinyume na sheria ya mtandao kifungu cha 23(1) na (2) namba 14 ya mwaka 2014.
MAHAKAMA KUU KUHUSU WALE WABUNGE 8 WA CUF…TAZAMA KWENYE HII VIDEO!!