Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mussa Taibu amesema hana taarifa za kukamatwa kwa Ofisa wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika himaya yake kama inavyosambazwa mitandaoni.
Kauli ya Kamanda Taibu imekuja siku moja baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuuambia umma kuwa Tito Magoti alikamatiwa eneo la Mwenge, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kamanda Taibu amesema kuwa amewasiliana na wenzake katika himaya yake, na hakuna mwenye taarifa za kukamatwa kwa mtumishi huyo wa LHRC ambaye alimakamatwa siku tatu zilizopita na bado haifahamiki anashikiliwa katika kituo kipi cha Polisi.
Magoti alichukuliwa Ijumaa iliyopita asubuhi na watu wasiojulikana wakiwa wamevalia kiraia eneo la Mwenge lakini jioni ya siku hiyo, Kamanda wa Polisi wa DSM, Lazaro Mambosasa alitoa taarifa akisema wanamshikilia pamoja na watu wengine watatu kwa uchunguzi wa tuhuma za jinai.
Kauli ya Kamanda wa Polisi wa Kinondoni imezidi kuibu utata juu ya sakata hilo kwani imekuja wakati watu wakisubiria tamko la Kamanda Mambosasa juu ya alipo Magoti, baada ya jana kusema kuwa ataweka wazi taarifa hizo leo.