Wananchi wa Vijiji vya Nyiboko, Borenga, Machanchari na Maremboto vilivyopo Kata ya Kisaka wilayani Serengeti wameliomba Jeshi la Wananchi (JWTZ) kukagua na kuondoa mabomu yaliosalia maeneo ya makazi baada ya Watoto kuokota bomu ambalo halijalipuka mara baada ya kuhitimisha mafunzo ya kivita.
Akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha Wananchi, Viongozi wa Serikali ya Vijiji vinne, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa JWTZ , Mzazi mmoja amesema Jeshi limekuwa likitumia eneo hilo kufanyia mazoezi, ambapo aliwaona Watoto wake wameshika bomu wakichezea na yeye akalichukua na kulitupa porini.
Mkuu wa Kikosi cha Makoko Kanali Samson Mshasha amesema ni kweli bomu hilo lilisahaulika ila amewaomba Wananchi wahame ili kujiweka salama, kwani 1996 Wananchi walikubali kutoa eneo kwa matumizi ya Jeshi ila kwa sasa wameanza kujenga nyumba (kutegesha) ili walipwe fidia kinyume na taratibu kwani kuna vifaa na silaha huwa zinabaki kwa bahati mbaya wakati wa mazoezi, pia amewataka Wananchi kutoa taarifa waonapo silaha na vifaa vingine vya kijeshi.
DC wa Serengeti Nurdin Babu, amesema kila Mwananchi aheshimu mipaka ya eneo la Jeshi na kuwataka waliokutwa na Jeshi wajitokeze watambulike ili utaratibu wa kuwalipa ufanyike ila waliotegesha nyumba ili walipwe hawatalipwa kwani ramani ipo na inaonesha vizuri.