Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho Thomas Thabane ameshtakiwa kwa mauaji ya mke wake Lipolelo Thabane mwaka 2017.
Mkewe wa sasa, Maesaiah, alishtakiwa kwa uhalifu kama huo mwaka jana kwani alikuwa akiishi na Bw Thabane wakati wa mauaji hayo na wanatuhumiwa kuajiri watu waliotekeleza shambulizi hilo. Wote wawili wamekana kuhusika.
Kesi hiyo imewashangaza wengi na kusababisha misukosuko ya kisiasa katika ufalme huo mdogo usio na bahari ambao umezungukwa kabisa na Afrika Kusini.
Maesaiah Thabane aliandamana na waziri mkuu huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82 hadi mahakamani. Alishtakiwa mwaka jana na kisha kuachiliwa kwa dhamana.
Mashtaka hayo yalisomwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu katika mji mkuu wa Maseru, badala ya chumba cha mahakama kuu, jambo ambalo si la kawaida.