Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameitaka Hospitali ya Rufaa Mwananyamala Jijini DSM kuacha mara moja tabia ya kuwatoza fedha kiasi cha shilingi elfu 75 akina mama wajawazito kwa ajili ya kujifungua bila ya kuwapatia ufafanuzi wa matumizi ya fedha hizo kwani sera na miongozo ya afya inawataka kutoa huduma hiyo bure.
Hayo yamebainika baada ya Waziri Ummy kutembelea hospitalini hapo kwa lengo la kuangalia utoaji wa huduma ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na ndugu wa wagonjwa waliofika hospitalini hapo kutibiwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Daniel Nkungu alieleza kuwa huduma zinazotolewa kwa mama na mtoto ni bure lakini wameweka huduma za haraka ambapo kwa watakaohitaji kujifungua ni shilingi elfu 75 na upasuaji ni shilingi laki 2 jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya ndugu wa wagonjwa kwamba kila mgonjwa anapofika hospitalini hapo ni lazima alipe kwanza Tsh. 75,000.
Waziri Ummy akatoa rai kwa wakazi wa Jiji la DSM kufuata taratibu za rufaa kabla ya kufika hospitalini hapo ili kupunguza msongamano wa wagonjwa lakini pia menejimenti isitumie huduma za haraka (first truck) kuwa kichocheo cha kuzorota kwa huduma za kawaida.